Friday 1 December 2023

ZAIDI YA ASILIMIA 100 YA WAVIU WANATAMBUA HALI ZAO-DC MASALA

 

Posted On: December 1st, 2023

MKUU WA WILAYA YA BUHIGWE KANALI MICHAELI MASALA AKIWASILI KWENYE ENEO LA HAFLA YA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI KIMKOA ILIYOFANYIKA KIJIJI CHA SONGAMBELE WILAYANI BUHIGWE DESEMBA MOSI, 2023.BAADHI YA WAKAZI WA  WILAYA YA BUHIGWE WALIOJITOKEZA KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI.

KAIMU MGANGA MKUU WA MKOA WA KIGOMA INNOCENT MSILIKALE AKITOA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA UKIMWI KWA MKOA WA KIGOMA WAKATI WA KILELE CHA MAADHIMISHO HAYO AMBAYO KIMKOA YAMEFANYIKA KATIKA HALMASHAURI YA BUHIGWE.

Asilimia 119.4 ya wanaoishi na Virusi vya UKIMWI mkoani Kigoma wanatambua hali zao huku wakiendelea kudumisha ufuasi wa dawa za kufubaza na kupunguza makali ya maradhi hayo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Masala alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo kimkoa yamefanyika katika kijiji cha Songambele wilayani Buhigwe.

Amesema katika kupambana na kudhibiti maradhi hayo, serikali imefanikiwa kuanzisha vituo 93 vya kutolea tiba na mafunzo kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI ikiwa ni sawa na Asilimia 97.9 ya mahitaji halisi kwa mkoa.

Sambamba na hayo, katika kukabiliana na virusi vya UKIMWI, Kanali Masala ameitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya tatizo la kuongezeka kwa uzito uliopitiliza pamoja na kujenga tabia ya kupima Afya mara kwa mara hali, itakayosaidia kubaini maradhi katika hatua za awali ikiwemo ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Aidha Kanali Masala amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu imedhamiria kuyatumia maadhimisho hayo kwa lengo la kutoa Elimu, Hamasa pamoja na kuongeza ushiriki wa Asasi za kiraia katika kuhakikisha huduma za VVU na UKIMWI zinayafikia makundi mbalimbali kwenye Jamii.

Akitoa Taarifa ya hali ya utekelezaji wa Afua za UKIMWI kimkoa, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Innocent Msilikale amesema kuanzia Januari hadi Oktoba 2023, jumla ya watu 409,785 wamepima VVU na kati yao 4105 kugundulika na maambukizi ya UKIMWI ikiwa ni sawa na Asilimia 0.93 ya waliopima.

Amesema katika kukabiliana na maradhi hayo mkoa umeendelea kuhakikisha huduma za upimaji wa VVU zinapatikana wakati wote, kutoa huduma ya tohara kwa wanaume, kutoa dawa kinga, kusajili wateja wenye VVU, kutoa mafunzo kwa watoa huduma za Afya ili kuwajengea uwezo katika kutoa Elimu kwa jamii.

Aidha Msilikale amezitaja Changamoto zinazoendelea kukinzana na utekelezaji wa Afua hizo kuwa ni baadhi ya wateja kuacha matumizi ya dawa na kujikita katika tiba mbadala hali inayosababisha kuzorota kwa Afya zao na hata kusababisha vifo.

Wakazi mkoani Kigoma wametakiwa kushiriki katika kupinga ukatilia dhidi ya wanawake na watoto kwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya makundi hayo ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

Wito huo umetolewa Leo Novemba 28,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli alipozungumza akimwakilisha Mkuu wa Mkoa kuzindua Kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa Mkoa wa Kigoma.

Amesema waathirika wakuu wa madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili wa kijinsia ni wanawake na watoto kutokana na jamii kutodhibiti tabia zisizozingatia usawa  wa kijinsia na haki za binaadamu kwa  makundi hayo.

‘’Tumeendelea kushuhudia vitendo vya utelekezaji wa familia, dhuluma katika mali za familia, ajira za watoto, unyanyasaji wa wanawake ndani ya ndoa pamoja na watoto wa kike kunyimwa haki zao za msingi katika familia na jamii kwa ujumla, mambo haya hayakubaliki na tunapaswa kuyapinga’’ amesema Kalli.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wanawake kutosita kujitokeza na kutoa taarifa kwa uongozi na vyombo vya usalama pale wanapokabiliwa na madhila yanayohusisha aina yoyote ya ukatili wa kijinsia.

‘’Baadhi ya wanawake wamekuwa wakibakwa hususani wakiwa katika maeneo ya mashambani lakini kutokana na kuogopa kuaibika au kutopewa kipaumbele kwa changamoto zao katika jamii, huamua kukaa kimya jambo linalohatarisha usalama wao wa Afya ya mwili na Akili’’ amesisitiza Kalli.

Kupitia Maadhimisho hayo yaliyoanza kitaifa Novemba 25  hadi Desemba 10, 2023, Mkuu wa Wilaya amewasisitiza wataalam kuhakikisha wanafika na kufikisha ujumbe wa maadhimisho  katika maeneo yote ya mkoa wa Kigoma hususani vijijini ambapo vitendo hivyo vimekithiri.

Akiwasilisha taarifa ya shughuli zinakazofanyika katika siku 16 za maadhimisho, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunuri amesema lengo mahususi la maadhimisho hayo ni kuungana na wadau ili kupata nguvu ya pamoja katika kuhimiza na kushawishi jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kufikia usawa.

Nzunuri amezitaja shughuli zinazofanyika kipindi cha kampeni ikiwa ni ufikishaji elimu na hamasa kupitia vyombo vya habari, kufanya mikutano na wananchi pamoja na kusikiliza kisha kutatua changamoto  zinazohusu ukatili wa kijinsia.

Aidha ameisisitiza jamii kuwekeza katika kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwa kuwa ni kundi ambalo linapitia changamoto nyingi ikiwemo mgawanyo wa majukumu katika familia, mila na desturi kandamizi, ukosefu wa ujuzi na umasikini.

Pia amebainisha changamoto nyingine zinazokabili kundi hilo ni  athari zitokanazo na changamoto za ubora na utoshelevu wa miundombinu nchini pamoja na ukubwa wa wategemezi katika kaya.

Kadhalika Nzunuri amesema matarajio ya Serikali pamoja na wadau ni kuhakikisha wanawake wanapata uelewa kuhusu masuala ya kijinsia, kupungua kwa idadi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na jamii kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

Upande wake Katibu wa Kamati ya Maridhiano ya Dini mkoa wa Kigoma Padre Castus Rwegoshora amesema upande wao kama wahudumu wa masuala ya kiimani wanaendelea kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimiana na kuchukualina  ili kudumisha hadhi na upendo kati ya wanadamu.

Pia ameishukuru serikali kwa kuendelea kutambua na kuchukua hatua dhidi ya changamoto ya uwepo wa vitendo vya ukatili miongoni mwa wanajamii.

Uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, umehudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Elisante Mbwilo, wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, viongozi wa Madhehebu ya Dini pamoja na wadau kutoka Taasisi za Umma na Binafsi.

No comments:

Post a Comment