Friday, 13 December 2013

Kigoma mhimili wa Uzalishaji chakula Kanda ya Magharibi

Shamba la zao la muhogo la kikundi cha wajasiliamali  Wilayani Kakonko.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda akikagua mavuno ya zao la mhogo katika shamba la wajasiliamali Wilayani Kibondo

Waziri wa Kilimo , Chakula na Ushirika Mhe. Mhandisi  Christopher Chiza akihutubia wananchi Mkoani Kigoma namna serikali ilivyojipanga kudhibiti ubadhilifu katika utoaji wa ruzuku ya pembejeo na utaoaji wake kwa muda mwafaka.


     Kigoma mhimili wa Uzalishaji chakula Kanda ya Magharibi  Kilimo ni sayansi inayojikita zaidi katika Uzalishaji wa mazao na ufugaji wa mifugo.  Nchi nyingi za Kiafrika hususani zinazopatikana kusini mwa jangwa la Sahara hutegemea kilimo kama uti wa mgongo ikiwemo Tanzania ambayo zaidi ya asilimia 80 ya wakazi hutegemea kilimo ili kuweza kujikimu na maisha yao ya kila siku.
     Nchi ya Tanzania yenye hali ya hewa nzuri kwa baadhi ya Mikoa ikiwemo Kigoma imekuwa ikijitahidi kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha kwa mwaka jambo ambalo linasaidia kutoa chakula kwa Mikoa ambayo haipati mvua za kutosha kwa musimu na kupelekea kukumbwa na baa la njaa.
       Makala hii, inaeleza kwa undani jinsi mkoa wa Kigoma uanvyojidhaatiti katika sekta ya kilimo ndani ya ambao una kila sababu ya kuitwa muhimili wa kilimo kwa Mikoa ya kanda ya magharibi mwa nchi ya Tanzania kwani kwa kiwango kikubwa umepiga hatua kadha katika Uboreshaji wa kilimo licha ya kukumbwa na changamoto.
       Mkoa wa Kigoma unakadiriwa kuwa na eneo linalofaa kwa kilimo la Hekta 2,668,630 na kati ya eneo hilo kiasi kinachotumika kwa kilimo  kwa sasa ni Ha 753,143.92  (sawa na asilimia 28.2). Kutokana na uwepo wa eneo la kutosha Mkoa unajitosheleza Kuzalisha chakula cha kutosha kwa kiwango kikubwa.
       Licha ya mafanikio makubwa ya kilimo Halmashauri za Mkoa wa Kigoma zinazidi kuweka malengo yake kwa mazao makuu manne ya chakula ya  Mahindi, Mpunga, Muhogo na Maharagwe kwa kuongeza Maeneo maalumu yenye hali ya hewa ya Kuzalisha mazao hayo manne ya chakula kutoka hekta 705,525 hadi Hekta 820,000 kwa msimu wa 2013/2014.
      Kutokana na mafanikio makubwa  ya kilimo katika Mkoa wa Kigoma, Mkoa umefanikiwa kuwa na akiba ya chakula katika kata ya Mtegowa noti iliyoko katika Wilaya ya Uvinza hali inyosaidia wakazi wa kata hiyo kupata msaada wa chakula kutokana na ukame uliotokea kutokana na mvua kukatika kuanzia mwezi Disemba hadi Machi mwaka 2013.
       Kama ilivyodokezwa hapo juu, kilimo huhusika pia na ufugaji wa mifugo maarufu kama (animal husbandry) kwa lugha ya kiingereza. Mkoa wa kigoma licha ya kuwa na eneo kubwa la wazi na Hifadhi bado una mifugo michache huku sababu kubwa ikiwa ni tatizo la mbung’o ambapo kutokana na takwimu kuna ng’ombe wapatao 155,443, mbuzi 498,087, kondoo 49,409, nguruwe 15,133 na kuku 876,150 japokuwa idadi hii inategemea Kuongezeka kutokana na Mazingira kuruhusu hali ya ufugaji.
    Nidhahiri kabisa kuwa  sekta ya mifugo bado haikidhi viwango stahiki katika Mkoa wa kigoma hali inayosababishwa na utoaji mdogo wa ruzuku kwa wafugaji. Serikali inalenga kuongeza katika sekta ya kilimo ili kuinua ufanisi wa ufugaji kama Nchi zingine ambazo hutegea ufugaji ikiwemo  Denimark na baadhi ya Nchi za mashariki ya mbali.
      Kama ilivyo katika jamii nyingine kama za kimasai zinazotegemea ufugaji, jamii ya watu wa Mkoa wa Kigoma hutegemea pia uvuvi kutoka ziwa Tanganyika ambalo huchukua kilomita 8,029, kwa kipindi kirefu limekuwa likiokoa maisha ya watu wanaoishi mwambao mwa ziwa hilo ambapo uvuvi katika ziwa hilo huchangia asilimia 95 ya mapato yote ya uvuvi huku maziwa madogo, mabwawa ya asili, mito na mabwawa ya kuchimba 127 yakichangia asilimia 5 ya mapato ya uvuvi ambapo samaki hao huuzwa ndani na nje ya nchi.
     Kwa upande mwingini, Vyama vya ushirika mkoani kigoma vimeongezeka ukilinganishwa na miaka iliyopita kwa sasa kuna jumla ya vyama vya Ushirika 255 vyenye jumla ya wanachama wapatao 49,395 huku vikiwa na akiba  ya jumla ya Tsh.4,465,171,657/= na hisa zake zikiwa  zenye thamani ya Tsh.512,568,044/=.
         Hivyo basi, kutokana na hali halisi ya sekta ya kilimo mkoa wa Kigoma, serikali kupitia watendaji wake inachuku hatua  stahiki ili kuweza kuinua na  kuboresha kwa kutatua matatizo kadha wa kadha kama kutoa ruzuku zisizo kuwa na riba yoyote wala gharama yoyote ili kuwapatia wakulima pembejeo za kilimo, kuongeza maafisa ugani wa kilimo na mifugo, kuboresha miundo mbinu ya usambazaji wa pembejeo, wataalamu kujihusisha na kilimo ili kutia chachu kwa wakulima wadogowadogo.

No comments:

Post a Comment