Mkoa wa Kigoma na mafanikio katika Sekta ya Afya.
Sekta ya afya ni sekta mhimu katika nyanja
zote za maisha ya mwanadamu. Hii ni kutokana na baadhi ya misemo ya wahenga
ambao hudiriki kusema kuwa “Mtu ni Afya”.
Hii ni dhahiri kuwa bila afya uhai wa mtu
au kiumbe chochote utakuwa matatani kwani afya ndio kichocheo cha mfumo mzima
wa utendaji wa shughuli zote za ndani na nje ya mwili wa mwanadamu.
Ebu
tumulike kurunzi letu katika sekta ya Afya ndani ya Mkoa wa Kigoma ambao kwa
takribani umepiga hatua katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo,Elimu
na nyinginezo.
Kwanza
kabisa napenda kuupongeza Uongozi wa Mkoa kwa kuonesha jitihada mbalimbali
katika kuboresha huduma za jamii kwa
kiwango fulani.
Mkoa
wa Kigoma wenye Jumla ya Hospitali sita huku tatu kati ya hizo zikimilikiwa na
serikali na tatu zikimilikiwa na mashirika ya dini, vituo vya kutolea huduma 247
ambapo sita kati ya hivyo ni hospitali, 22 ni vituo vya afya na zahanati zikiwa
219 umekuwa katika mchakato wa kuimarisha vituo hivyo ili kuweza kutoa huduma zenye
tija kwa wanajamii.
Katika Uboreshaji huo
unaolenga kutoa na kuweka Mazingira bora ya kufanyia kazi kwa Watumishi, vituo
vingi vya serikali vinajenggwa na kuimarishwa kupitia fedha za ujenzi na
ukarabati wa vituo vya kutolea huduma(JRF) na Mfuko wa Maendeleo ya Afya ya
Msingi(MMAM).
Je,
licha ya serikali kuwa na Mpango na adhma ya kuboresha vituo vya kutolea huduma
za afya, huduma zinazotolewa zinakidhi idadi na ubora wa huduma hizo?
Hii inawezekana jibu lake lipo katika kauli
mbiu ya serikali ya Awamu ya nne yenye Mpango wa kuwepo kwa zahanati kila
kijiji na Kituo cha afya kwa kila Kata ambapo kwa dhana hiyo, Mkoa una upungufu
wa zaidi ya zahanati mpya 38 na vituo vya afya 98.
Hata
hivyo, licha ya afya kuwa muhimu sana, bado Mkoa unaupungufu wa Watumishi
katika hospitali za Wilaya na Mkoa ambapo hospitali zote hizi zina Jumla ya
Watumishi 955 wa kada zote ambapo Watumishi wanao hitajika kulingana na Ikama
ni 2747 ambayo inonesha kuwa idadi ya Watumishi waliopo ni asilimia 34.7.
Jitihada za makusudi zimeendelea kuwekwa
hali inayoonesha Ufanisi mkubwa hususani katika kuupiga vita ugonjwa wa Malaria
na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ambapo kulingana na matokeo ya Malaria na
UKIMWI (THIMS 2011/2012) uliofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu unaonesha kuwa
Mkoa wa Kigoma unakiwango cha maambukizi asilimia 3.4 kulingana na wastani wa
Kitaifa wa asilimia 5.1 hali inayoashiria Ufanisi na mafanikio makubwa
unaofanywa na sekta ya afya katika Mkoa wa Kigoma.
Sambamba na hilo, huduma za UKIMWI zinatolewa
katika vituo vyote vya Mkoa wa Kigoma
kupitia Halmashauri zote ambapo Kigoma Ujiji vipo 21, Kigoma Vijijini 76,
Kasulu 77 na Kibondo 63 huku serikali na watu binafsi kama wakihusika katika utoaji wa huduma hizo zoezi
ambalo huonesha Ufanisi mkubwa katika sekta ya Afya Mkoani Kigoma.
Katika kuleta ubora wa hali ya juu katika
sekta ya Afya ndani ya Mkoa wa Kigoma , vita dhidi ya Malaria katika vituo vya
Afya imeshika kasi ambapo Takwimu kutoka katika vituo vya Afya zinaonesha kuwa
bado Malaria inaenea kwa kasi japo Mpango wa kusambaza vyandarua vya bure kila
Nyumba umefanikiwa.
Ili kuweza kujibu maswali na kuepukana na
Matatizo yasiyokuwa ya lazima katika sekta ya Afya , serikali kupitia wadau
mbalimbali inadhamiria kuweka sera nzuri itakayo ongeza idadi ya Watumishi wa
Afya, sera itakayo andaa Mazingira mazuri ya kufanyia kazi kama ujenzi wa
Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali.
No comments:
Post a Comment