Monday, 9 June 2014

Ufugaji wa nyuki wawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Kigoma




Ufugaji wa nyuki wawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Kigoma
Ufugaji wa nyuki umekuwa ukipigiwa kampeni sana na viongozi wa nchi hapa Tanzania hasa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ambaye pia ni mdau nambari moja katika sekta ya Ufugaji nyuki.

Ufugaji wa nyuki unaelezwa kuwa na faida nyingi ambazo hugusa maisha ya mwanadamu kwa njia moja ama nyingine, sambamba na kutupatia mazao ya asali na nta, nyuki pekee ni viungo muhimu katika kutunza mazingira, pamoja na kusaidia uchavushaji wa mimea na mazao shambani. 
Mizinga ya nyuki ya Kisasa inayotumiwa na wananchi wa Mkoa wa Kigoma.

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa maarufu kwa ufugaji wa nyuki nchini Tanzania, ukiacha Mikoa ya Katavi, Rukwa, na Kagera. Ufugaji wa nyuki ni shughuli ya asili mkoani Kigoma hali hii inatokana na uwepo wa aina nyingi za mimea na misitu ya asili ya miombo inayotoa aina nyingi za maua ambayo ni kivutio kikubwa kwa nyuki.

Hapo awali ufugaji wa nyuki haukupewa kipaumbele kama ni shughuli inayoweza kumuingizia mfugaji wa nyuki kipato chenye tija. Kwa miaka ya hivi karibuni sekta ya ufugaji wa nyuki imepewa msukumo mkubwa kitaifa na kimkoa hivyo kuifanya shughuli ya ufugaji wa nyuki na kuwa ya manufaa kwa jamii kiuchumi na lishe.

Shughuli ya ufugaji wa nyuki inafanyika katika wilaya zote za mkoa wa Kigoma na imeendelea kukua mwaka hadi mwaka ikihusisha jinsia zote. Hadi kufikia mwaka 2013/2014 idadi ya wafugaji wa nyuki Mkoani Kigoma ni 3,543 miongoni mwa hao  wanawake wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki ni 831.

Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akikagua mizinga ya nyuki ya kisasa iliyofadhiliwa na Serikali ya Ubeligiji kupitia shirika la maendelo la nchini humo.


Katika kuhakikisha sekta ya ufugaji nyuki Serikali inashirikiaa na wahisani mbalimbai ili kuwawezesha wananchi kuifanya skta hii kuwa ya kibiashara zaidi kitaifa na kimataifa. Aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la mizinga ya kisasa 6,357 iliyofadhiliwa na wahisani ktoka Nserikali ya Ubelgiji, mizinga ya asili ambayo haileti tija katika uzalishaji inazidi kupungua ambapo hadi sasa kuna jumla ya mizinga ya asili 110,252.

Ili kuhakikisha kuwa sekta ya ufugaji Nyuki inachangia kikamilifu katika jitihada za kuondoa umaskini na katika pato la Taifa, Serikali ya Mkoa imeendelea kuwapa elimu na kuwahamasisha wananchi kujishughulisha na ufugaji wa nyuki.

Mwaka 2007 mwezi Agosti hadi mwezi Juni, 2011 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji ilianzisha na kutekeleza Mradi wa kuendeleza ufugaji Nyuki kwa kuboresha uchakataji, kutafuta masoko ya asali, nta na mazao mengine ya nyuki katika Wilaya za Kibondo na Kigoma ambapo jumla ya Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia saba (1,700,000,000/=) zilitumika.

Mradi huo umesaidia sana kuongeza ubora wa asali na kiasi kinachozalishwa kwa mwaka ambapo uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka tani 100 mwaka 2007 hadi tani 345.6 mwaka 2012, na nta chini ya tani 5 mwaka 2007 hadi kufikia wastani wa tani 10 mwaka 2011.

Kutokana na mafanikio ya mradi huo katika awamu ya kwanza, Wafadhili wa Mradi huo Serikali ya Ubelgiji walikubali kuongeza awamu ya pili ya Mradi huo ya miaka minne katika Wilaya za awali za Kibondo na Kigoma.
 Aidha, Wilaya ya Kasulu imeongezwa kwenye mradi huo katika awamu ya pili ambao ulianza rasmi mwezi Mei, 2012. Mradi huu katika awamu ya pili umepangwa kutumia kiasi cha Uro milioni 2.8 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 5.6.

Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akikagua asali na bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wajasiliamli wanaojishughulisha na Ufugaji wa nyuki Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.

No comments:

Post a Comment