Tuesday, 29 November 2016

Zaidi ya Wanafunzi 17,854 kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2017 Mkoani Kigoma

Jumla ya wanafunzi 17,854 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2017, kati yao wavulana ni 9931 na wasichana 7923 Kati ya wanafunzi hao wanafunzi watakaosoma shule za Bweni ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma ni 92 na sekondari za kutwa ni 17,762.

Watahiniwa 19,062 kati yao wavulana 10,738 na wasichana 8,324 ambao ni sawa na asilimia 70.79 walifaulu Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2016  uliofanyika tarehe 07 – 08 Septemba, 2016 katika Mkoa wa Kigoma  kwa kupata alama kati ya 100 na 250. Ufaulu huo ni ongezeko la silimia 16.75 ukilinganisha na ufaulu wa asilimia 54.04 kwa watahiniwa wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2015. 

Akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Mitihani wa Mkoa katika kikao cha kutangaza Majina ya wanafunzi waliochaguliwa kuendeleza na kidato cha kwanza Januari 2017, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Moses Msuluzya alisema Ufaulu huo umeufanya Mkoa wa Kigoma kushika nafasi ya 11 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Msuluzya aliongeza kuwa Ufaulu huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na walimu kujituma, usimamizi madhubuti wa Halmashauri na Mkoa.  Aidha, utoaji wa Elimu bila malipo kuanzia Elimu ya Msingi hadi kidato cha Nne pia umechangia ongezeko la ufaulu katika Mtihani huu.

Aidha Wanafunzi 1208 wakiwemo wavulana 807 na wasichana 401 wenye alama za ufaulu kuanzia 100 wamekosa nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2017 kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. 

Hata hivo wanafunzi hao 1208 watachaguliwa kuingia kidato cha kwanza ifikapo Februari, 2017 baada ya Halmashauri kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kuweza kuchukua wanafunzi hao waliobaki.  Halmashauri ambazo wanafunzi waliofaulu lakini wameshindwa kupata nafasi kuingia kidato cha kwanza ni Kasulu Mji wanafunzi 568 na Uvinza wanafunzi 568. 

Aidha Msuluzya alitoa wito kwa wazazi/walezi na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kuanza masaomo maramoja ifikapo Januari, 2017.  Hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayekwamisha au kuzuia mwanafunzi aliyechaguliwa kuendeleza na masomo ya sekondari.

Kuhusu suala la madawati Msuluzya amewakumbusha kuwa wahakikishe kila mwanafunzi aliyechaguliwa na anayeendelea na masomo anakaa kwenye dawati kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Aidha, zoezi la utengenezaji madawati, viti na meza litakuwa endelevu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma na hakuna ruksa ya kuchangisha mchango katika shule za Msingi na Sekondari.


Mkoa wa Kigoma ulikuwa na watahiniwa 27,111 kati yao wavulana 13,574 na wasichana 13,537 waliokuwa wamesajiriwa kufanya mtihani.  Watahiniwa waliofanya mtihani huo Septemba, 2016 ni 26,928 kati yao wavulana ni 13,468 na wasichana 13,460.  Watahiniwa 183 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ugonjwa na vifo.

No comments:

Post a Comment