Wednesday 14 May 2014

Jumla ya Miradi 62 yenye Gharama ya Tshs 10,772,927,756.65 yazinduliwa, kuwekewa mawe ya Msingi, na mingine kufunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014 Mkoani Kigoma



 Jumla ya Miradi 62 yenye Gharama ya Tshs 10,772,927,756.65 yazinduliwa, kuwekewa mawe ya Msingi, na mingine kufunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014 Mkoani Kigoma.
Mwenge wa Uhuru ni ishara ya Amani, Upendo, Umoja, Heshima na Mshikamano wa Kitaifa. Pia, Mwenge wa Uhuru katika historia yake umekuwa kichocheo kikubwa cha Maendeleo ya Taifa letu. Hivyo, ni dhahiri kwamba Mwenge wa Uhuru ni ishara ya Uhai na Nguvu ya Taifa ambayo leo hii iko Mkoani kwetu
Ukiwa katika Mkoa wa Kigoma Mwenge wa Uhuru unaendelea kukimbizwa na utakimbizwa katika Wilaya sita (6) ambazo ni Kakonko, Kibondo, Kasulu, Buhigwe, Kigoma na Uvinza zenye Halmashauri saba (7) moja ikiwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Mwenge wa Uhuru unapokelewa Mkoani Kigoma tarehe 10 Mei, 2014 ambapo utakimbizwa kwa jumla ya siku saba (7). Baada ya kupokelewa, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa na kukesha katika Wilaya ya Kakonko. Kuanzia tarehe 11 hadi 16 Mei, 2014 Mwenge huo utakimbizwa na kukesha katika Wilaya za Kibondo, Kasulu, Buhigwe, Kigoma, Manispaa ya Kigoma/Ujiji na Wilaya ya Uvinza. Tarehe 17 Mei, 2014 asubuhi Mwenge utapelekwa kukabidhiwa Mkoa wa Katavi.

Wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Kigoma mwaka 2014,umefanya shughuli za kuweka mawe ya msingi, kufungua, kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo iliyojengwa au kukarabatiwa na Wananchi kwa kutumia nguvu zao, mchango wa Serikali za Mitaa, Serikali Kuu na Wahisani.

Katika Mkoa wa Kigoma, Mwenge wa Uhuru utapitia jumla ya Miradi 62 yenye thamani ya shilingi bilioni kumi mia saba sabini na mbili milioni mia tisa ishirini na saba elfu mia saba hamsini na sita na senti sitini na tano. (10,772,927,756.65). Kati ya miradi hiyo, Miradi 11 yenye thamani ya Shilingi 893,270,314/= ipo Wilaya ya Kakonko. Miradi 11 yenye thamani ya Shilingi 972,143,983,/= ipo Wilaya ya Kibondo, na miradi 8 yenye thamani ya Shilingi 1,226,938,473,/=  ipo Wilaya ya Kasulu.

Kati ya miradi 62 Wilaya ya Bugigwe inamiradi 11 yenye thamani ya Shilingi 2,528,160,135/=, Wilaya ya Kigoma miradi 7 yenye thamani ya Shilingi 1,423,722,877/=, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji kuna miradi 7 yenye thamani ya Shilingi 3,221,991,974/=. Miradi 7 yenye thamani ya Shilingi 506,700,000/= ipo katika Wilaya ya Uvinza.

Kwa mwaka huu 2014, Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Kigoma zitazindua jumla ya Miradi 20 na Kufungua miradi 8. Miradi itakayowekewa mawe ya msingi ni 17 na miradi itakayotembelewa na kukaguliwa ni 8. Miradi 9 itakuwa ya uwezesho wa vikundi vya Wajasiliamali Wanawake na Vijana.

Kati ya Shiling 10,353,661,791.05/= ambayo ni thamani ya miradi yote 62 itakayohusika katika Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014 Mkoani Kigoma, 7% sawa na Shilingi 782,025,966/= ni mchango wa nguvu ya wananchi. Serikali Kuu imechangia Shilingi 4,896,196,773/=  sawa na 46% wakati  6% sawa na shilingi 647,930,064/= ni mchango wa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma. Mchango wa Wahisani ni Shilingi 4,446,774,954/= sawa na 41%.


















Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Bi. Rachel Stevene Kassanda akiendesha trekta kama ishara ya kukabidhi kwa kikundi cha vijana wajasiriamali  Wilayani Kasulu.

Uzinduzi wa Madaraja manne Wilayani Kasulu.
Uzinduzi wa Maabara katika Sekondari ya Kanyonza Wilayani Kakonko.

No comments:

Post a Comment