Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewaonya waajiri katika Sekta za Umma na
binafsi mkoani hapa kuachana tabia ya kuwanyanyasa watumishi na kufuata
miongozo ya kazi zao ili kulinda haki na
stahiki za watumishi walio chini yao.
Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza na
wafanyakazi wa Mkoa wa Kigoma kwenye
kwenye Hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani (Mei
Mosi) iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Amesema ni vizuri Menejimenti za Taasisi zikajiwekea utaratibu wa kukutana
na viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi na kuweka mipango ya pamoja badala ya
kuviona vyama hivyo kuwa ni maadui na kuvifanya kuwa daraja muhimu baina ya
waajiri na waajiriwa.
Vyama vya wafanyakazi visibebe jukumu la
kusimamia maslahi ya watumishi pekee bali vijikite pia katika kutoa Elimu ua
kanuni na Sheria kwa watumishi pekee
bali vijikite pia katika kutoa Elimu ya Kanuni na Sheria kwa watumishi
sambamba na kujenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara na pande zote
mbili yaani waajiri na waajiriwa ili kutatua changamoto zao.
‘’mitazamo ya kujikita upande mmoja imekuwa
ikichangia sana kukuza migogoro baina ya watumishi na waajiri wao hali
inayochangia uzoroteshaji wa matokeo chanya katika utendaji kazi na kushindwa
kutoa huduma bora kwa wananchi’’ amesema.
Pia Andengenye amewataka watumishi kuendelea
kupiga vita uvivu, rushwa, kuepuka vitendo vya utovu wa nidhamu, ubinafsi na
kuongeza bidi na maarifa mapya katika utendaji kazi ili kuimarisha uchumi wao
binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Andengenye amewasisitiza
watumishi wa Uma mkoani Kigoma kuendelea kuziamini taasisi rasmi za kifedha kwa
kujiimarisha kiuchumi na kutimiza malemgo yao kupitia mikopo inayotolewa na
Taasisi hizo huku akiwataka watendaji katika Taasisi hizo kuendelea kupunguza
riba za mikopo ili watumishi waweze kurejesha fedha wanazokopa kwa muda muafaka.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa
amewakumbusha watendaji hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha
wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa
ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kugombea katika nyadhifa mbalimbali
katika nafasi za uongozi.
Andengenye amewaasa watumishi kuendelea kufanya
mapinduzi ya kifikra sambamba na kuongeza juhudi, nidhamu na maarifa katika
utendaji kazi wao wa kila siku.
Akisoma risala
kwa mgeni rasmi Katibu wa
Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi mkoa wa Kigoma Jumanne Hamis ametoa wito
kwa wafanyajkazi wote nchini kuongeza juhudi katika kufanya kazi zao huku
wakizingatia weledi.
Aidha kiongozi huyo ameiomba serikali
kuwatazama upya baadhi ya wastaafu
kutokana na kulipwa kiasi cha fedha kisichoweza kukidhi mahitaji yao ya
kimasisha, kushauriana na Taasisi za kibenki ili ziweze kupunguza riba katika
mikopo wanayotoa kwa watumishi pamoja na kuchukua hatua kali kwa baadhi ya
waajiri katika Taasisi binafsi kutokana na kushindwa kuzingatia sheria ya
ulipaji wa mishahara kwa ngazi ya kima cha chini.
Kadhalika ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Samia
Suluhu kwa kupandisha madaraja ya mishahara kwa watumishi wa Umma, kuondolewa kwa tozo ya
Asilimia Sita kwenye mikopo ya Elimu ya Juu, kuongeza umri wa wategemezi kutoka umri wa miaka 18
hadi 21.
Aidha pongezi hizo zimehusisha serikali
kushughulikia maslahi ya watumishi
walioondolewa kazini kwa kugushi vyeti pamoja na kulipa madeni ya mishahara ya
walimu.
Kupitia hotuba hiyo, Katibu huyo ameiomba
serikali kurejesha kikokotoo cha Asilimia Hamsini kwa moja chini ya mia tano
arobaini kwa mshahara wa mwisho badala ya kutumia mfumo wa kutafuta mshahara
bora wa miaka mitatu ya utumishi.
Aidha ameiomba serikali kufuatilia utendaji
kazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao
wa kisheria wa kufuatilia michango ya watumishi kwa waajiri na kusababisha
changamoto na mgogoro mkubwa baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi kimkoa kwa
mwaka 2024 yamefanyika katika Halmashauri ya Mji Kasulu yakiwa na kaulimbiu isemayo ‘’Nyongeza ya
Mishahara ni msingi wa kuongeza ufanisi na Tija katika utoaji wa Huduma na
uzalishaji mali kwa ajili ya Maendeleo ya Jamii’’